UJA UNA UZITO

UJA UNA UZITO

Swala moja tatanishi, latia chungu moyoni,
Wali wa daku upishi, utu uso madhumuni,
Dira hatuna waashi, kupoteza ‘tamaduni,
Jengo letu ‘tamaduni, tazama laporomoka!

Tazama laporomoka,hatuna ustaarabu,
Vipusa twajianika, kwa kujitia adhabu,
Kwa mapenzi kukwazika,’patapo mimba ghadhabu,
Jengo letu utu nzima, tazama ndugu mchanga..

Tazama ndugu mchanga, kuavya ni mazoea,
Wafu ‘mekuwa wachanga,utovu moyo kulea,
Uovu watia nanga, vitoto vinapolia,
Jengo letu utu nzima, tazama janga ni hili.

Tazama janga ni hili,lasababisha majuto,
Laana kubwa jabali,kuavya huyo mtoto,
Ya muhimu kujadili,uhai kweli ni wito,
Dhamira yako kidosho, usitupe kwenye moto.

Usitupe kwenye moto, dhamana yako muhimu,
Kwani zawadi mtoto, kwako kutunza ni zamu,
Tumaini lako ndoto, yeyote usilaumu,
Usiavye ni haramu, mimba katu si jiwe!

Mimba katu si jiwe, ni kiumbe cha Mungu,
Ni kwa nini auliwe, hidaya kutoka mbingu,
Matabibu na wajuwe, uadilifu wa uwingu,

Tusiishi kwa machungu,ni madhara hadharani.

Ni madhara hadharani,ni ombi la kuwa tasa,
‘Kichunguza kwa undani, uzao utaukosa,
Tabia mbi la utani, tazama kisa makosa,
Jengo letu utu nzima, waashi tusimamishe.

Na mengi tusofahamu, dhana zetu kawaida,
Si utumwa kuheshimu, kuwa mama, kina dada,
Tudhamini kujikimu, aidha omba msada,
Nasaba ni muhimu, furaha ya aushini.

Kwa heri nawapungia, kitabu weka jalada,
Pazuri twaelekea, mkazo kutilia mada,
La hasha! Sitolegea, taji tupate shahada,
Kuimarisha asili yetu, kuwa ‘Mama’ ni jukumu.

JOY RITA.2019.

3 thoughts on “UJA UNA UZITO

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *